Ijumaa , 16th Apr , 2021

Mdau wa Elimu nchini Richard Mabala amesema kuna haja ya Serikali kupitia Wizara ya Elimu na idara zake mbalimbali kupitia upya mifumo ya elimu na ufundishaji ili kuiboresha kwa manufaa ya wanafunzi wanaopita kwenye mifumo hiyo.

Mdau wa Elimu nchini Richard Mabala

Mabala ameyaeleza hayo leo kwenye mahojiano na kipindi cha Supa Breakfast cha East Africa Radio, ambapo ametolea mfano namna wanafunzi wa shule za awali na msingi wanavyolazimika kutumia muda mwingi zaidi darasani kuliko uhalisia wa mahitaji ya elimu yao.

''Tukianza kwenye shule za awali wanasoma kama wanafunzi wa chuo kikuu, wanakaa kwenye madawati siku nzima. Mtoto mdogo anatakiwa kucheza kupanua ubunifu wake na uwezo wa kuchambua mambo,'' amesema Richard Mabala.

Aidha amesema mfumo wa sasa unamnyima mwanafunzi wigo mpana wa kuwa mbunifu ndio maana wahitimu wengi hata wale wa elimu ya juu wanashindwa kujiari.

''Tukiangalia kwa sasa kwenye mfumo wetu wa elimu, ubunifu unafundishwa wapi katika elimu yetu? Kwahiyo ni lazima tuangalie upya ili kuboresha uwezo wa wahitimu wetu,'' ameeleza.