Alhamisi , 16th Feb , 2017

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limetoa taarifa ya kukamatwa kwa jumla watuhumiwa 349 akiwemo 'video queen' Agnes Gerald maarufu kwa jina la 'Masogange', katika oparesheni ya kuwasaka watu wanaohusika na dawa za kulevya

Kamishna Simon Sirro

 

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro amewaambia waandishi wa habari kuwa kati ya watuhumiwa 349, watuhumiwa 17 akiwemo mrembo anayepamba video za muziki za wasanii Agnes Gerald maarufu kama Masogange watarajiwa kupandishwa kizimbani kwa tuhuma za kutumia dawa za kulevya na kwa sasa bado wapo chini ya uangalizi wa polisi.

Hadi sasa watuhumiwa 16 wamekwisha fikishwa Mahakamani, huku majalada 24 yamekwisha peleke kwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ambapo muda wowote watuhumiwa hao watapandishwa kizimbani kujibu tuhuma hizo huku uchunguzi ukiendelea juu ya watuhumiwa wengine.

Mbali na watuhumiwa hao, Jeshi Kanda Maalum ya Dar es Salaam pia limefanikiwa kukamata jumla ya kete 612 za dawa za kulevya aina ya heroin, puli 816 na misokoto ya bangi 89 pamoja na mabunda 19 ya mirungi.

Aidha, Jeshi hilo pia linamshikilia kijana mmoja mwenye umri wa miaka 23 Omari Abeid Bakari ambaye ni manafunzi na mkazi wa maeneo ya JKT Mgulani, kwa tuhuma za kusambaza taarifa za uongo mitandaoni akiwahusisha viongozi wakuu wa kisiasa, wakidini na watu mashuhuri ambapo Kamishna Sirro ametoa tahadhari kwa wananchi kuacha mara moja kutoa taarifa za oungo mitandaoni kwani hawata sita kuwachukulia hatua za kisheria.

Kuhusu askari 9 kati ya 12 waliotuhumiwa kuhusika na dawa hizo, Kamanda Sirro amesema askari hao watapelekwa kwenye tume ya maadili kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kisheria.