Ijumaa , 25th Sep , 2020

Wakazi wa jiji la Dar es salaam, wameomba kuzibwa haraka kwa chemba ya maji taka ambayo imepasuka katika barabara ya Bibi Titi iliyopo Posta ambayo licha ya kuhatarisha usalama wa watumiaji wa barabara hiyo lakini pia inaleta athari za kiafya kwa wakazi wa maeneo hayo.

Pichani ni chemba ya maji taka ambayo imepasuka katika barabara ya Bibi Titi iliyopo Posta Dar es Salaam.

Wakiongea na EATV leo wakazi hao wamesema maji yanayotiririka kutoka kwenye chemba hiyo yanatoa harufu mbaya huku pembezoni mwa chemba hiyo kukiwa na wafanyabiashara wa chakula jambo ambalo kiafya ni hatari.

“Chemba hii ina takribani mwezi sasa tangu ilipoanza kutiririsha maji taka na wahusika wanapita na kuiona hali hii lakini hakuna hatua zozote zinazochukiliwa” amesema mmoja wa wakazi hao Abdallah Juma.

Wamesema hatari nyingine iliyopo ni kuharibika kwa barabara kwa sababu maji hayo machafu yanatuhama kwa muda mrefu hali inayosababisha miundombinu ya barabara hiyo kuharibika na kutishia usalama wa vyombo vya usafiri vinavyotumia barabara hiyo.