Ijumaa , 26th Feb , 2021

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Simon Sirro, amewataka wale wote wanaofanya uhalifu kwa kutumia silaha kuhakikisha kabla hawajatoka majumbani mwao wahakikishe wameziaga familia zao kwani jeshi hilo haliwezi kuwavumilia.

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Simon Sirro

Kauli hiyo ameito hii leo Februari 26, 2021, mara baada ya Rais Dkt. John Magufuli, kuzindua Chuo cha Maafisa wa Polisi Kurasini Dar es Salaam, ambapo alitumia nafasi hiyo kutoa taarifa ya mwenendo wa uhalifu hapa nchini na kusema kuwa hali ya usalama ni shwari licha ya uwepo wa changamoto.

"Watanzania na wahalifu watuelewe awamu hii si ya kuendekeza ujambazi wa kutumia silaha na ugaidi, ukiingia kwenye hii biashara usiilaumu serikali, kwahiyo Mh. Rais nikuhakikishie wale ambao hawataki kubadilika tutawalazimisha," amesema IGP Sirro

Aidha, IGP Sirro ameongeza kuwa, "Huwa nasema kabla hujachukua bunduki yako nyumbani kwako kwenda kusumbua Watanzania uage familia yako kwa sababu habari ya bunduki ukamataji wake huwa ni mgumu, Watanzania walishasahau benki zao kunyang'anywa fedha".