Jumanne , 28th Mar , 2017

Baadhi ya wachimbaji wadogo ambao wanadai kuwa ni sehemu ya wamiliki wa makontena yaliyozuiliwa katika bandari ya Dar es Salaam yakiwa na shehena ya mchanga wa madini, wameiomba serikali kupitia upya zuio hilo kwa maelezo kuwa limeathiri biashara.

Wachimbaji wadogo wadogo wanaosafirisha nje ya nchi mchanga wenye masalia ya madini wakizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam hii leo

Wakizungumza katika mkutano na wanahabari leo Jijini Dar es Salaam, wachimbaji hao wamesema kimsingi hawapingani na uamuzi huo wa serikali bali wanaunga mkono kwani uamuzi huo unaotokana na agizo la Rais John Pombe Magufuli alilolitoa takribani mwezi mmoja uliopita, linayalenga makampuni makubwa na siyo wao ambao ni wamachinga kwenye sekta ya madini.

Wamesema tangu lilipotolewa agizo la kutosafirisha nje mchanga wenye masalia ya madini, wamekuwa wakipata hasara kubwa ambapo mmoja wa wachimbaji hao amesema anaingia hasara ya zaidi ya shilingi milioni nne kwa siku kutokana na kusitisha shughuli za uchimbaji huku akitakiwa kulipia wastani wa dola ishirini kama gharama ya utunzaji kwa kila kontena linaloshikiliwa pale bandarini.

Sehemu ya makontena ya mchanga yanayoshikiliwa bandarini

Kwa mujibu wa maelezo ya wachimbaji hao akiwemo Bw. Mohammed Mkwayu anayemiliki kampuni ya Kambi Mineral Resources inayofanya shughuli zake wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma na Bw. King Selemani anayemiliki kampuni ya Wit Mining inayofanya shughuli zake wilaya za Kongwa na Mpwapwa; zaidi ya kontena sitini za wachimbaji wadogo wadogo zimezuiliwa zisisafirishwe kwenda nje ya nchi na kwamba hatua hiyo imechukuliwa huku wakiwa na vibali vyote vinavyowaruhusu kufanya biashara hiyo.