Jumanne , 24th Nov , 2020

Wabunge wateule wa viti maalum kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wakiongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa CHADEMA Halima Mdee, wamekula kiapo hii leo katika viwanja wa Bunge jijini Dodoma.

Wabunge wa viti maalum wa CHADEMA wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kula kiapo cha ubunge, kilichoongozwa na Spika Ndugai.

Zoezi la uapisho wa wabunge hao limeongozwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, hii leo Novemba 24, 2020.

Akizungumza mara baada ya kula kiapo, Halima Mdee amesema kuwa, "Nikishukuru chama changu cha CHADEMA kikiongozwa na Mwenyekiti wetu Freeman Mbowe, ambao kupitia wao sisi tumepata nafasi ya kukiwakilisha chama chetu, viti hivi siyo hisani ila ni sehemu ya ushindi mkubwa ambao chama chetu kilipata".

"Mh. Spika tumefanya kazi wote kwa miaka zaidi ya 10, tutafanya kazi kwa uaminifu kama Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa uadilifu mkubwa, tuna vijana wapya sisi kama dada zao tutahakikisha wanafanya kazi nzuri kwa ajili ya Taifa hili", ameongeza.

Waliokula viapo hivyo hii leo ni wabunge 19, akiwemo Ester Bulaya, Salome Makamba, Grace Tendega, Kunti Majala, Esther Matiko, Halima Mdee, Cecilia Paresso, Agnesta Lambati, Nusrat Hanje, Jesca Kishoa, Tunza Malapo, Konchester Leonce Rwamlaza.