Ijumaa , 30th Sep , 2022

Viongozi wa dini nchini wametaka elimu kuhusu masuala ya haki za binadamu kuwafikia zaidi wananchi katika ngazi ya familia, ili kupunguza kukithiri kwa matukio ya ukatili na uvunjifu wa haki za binadamu nchini.

Viongozi wa madhehebu mbalimbali nchini

Hayo yamebainishwa Wakati wa kikao cha viongozi wa dini zote kilichoenda sambamba na uzinduzi wa  kitabu kitakacho kuwaelimisha watu kuhusu umuhimu wa haki za binadamu huku  Askofu Mkuu wa Monnonite Nelson Kisare akitaka viongozi wa dini katika jamii zao kuzijua sheria na haki za binadamu ili waweze kutoa zaidi elimu kwa wananchi wanaowaongoza.

Aidha viongozi hao Wamekemea baadhi ya viongozi wa dini na viongozi wengine kwenye jamii ambao wamekuwa wakifanya vitendo vya ukatili na uvunjifu wa haki za binadamu, huku Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu Bakwata Sheik Khamis Mataka akitaka nao wawajibishwe na sheria zilizowekwa.

Kwa upande wao Mratibu wa Mtandao wa watetezi Haki za binadamu Onesmo Ole Ngurumo  Tanzania ametaka jamii kwa ujumla kushikamana katika kupinga uvunjwaji wa haki za binadamu, na kuacha kuwaachia wanaharakati pekee kupambania watu kupata haki zao, akihimiza watoto pia kufundishwa kuzijua haki za binadamu.