Jumatatu , 21st Sep , 2020

Wakati vijana wengi wasomi wakiendelea kuhangaika na ajira rasmi katika taasisi na kampuni wapo wengine walioona fursa katika ujasiriamali licha ya changamoto ya masoko na mitaji.

EATV imekutana na kikundi cha wasichana watatu ambao wote ni wahitimu wa vyuo mbalimbali Jijini Dar es Salaam baada ya kukosa ajira zinazoendana na taaluma yao wakaamua kuungana na kufanya ujasiriamali wa uuzaji wa bidhaa za nguo, viatu na vito vya thamani.

“Sisi tulianza kidogo kidogo kuanzia chuoni na hii ilitokana na wengi waliotupiata madarasa kuzidi kulalamikia kukosa ajira mtaani, tumejiendeleza mpaka sasa hivi hatuwezi kulalamika kwakweli yinayaona mafanikio”alisema Liliani Ludovick mjasiriamali

Licha ya kuanza biashara hiyo ambayo kwa kipindi kirefu wamekuwa wakifanya kwa njia ya mtandao wanasema suala la mitaji na mwamko kutoka kwa wazazi kukubali wao kufanya biashara limekuwa ni changamoto kubwa huku wakitoa wito kwa wasomi wengine kuchangamkia fursa zilizopo.

“Kiukweli wazazi mwanzoni hawakupendezwa na jambo hili haswa baada ya kuwa na mategemeo makubwa katika masomo yetu wakitegemea kuwepo katika ajira rasmi, ila baadae walielewa na sasa wanatupa motisha kusonga mbele tunaamini ipo siku tutamiliki maduka makubwa “ alisistiza Marietha Mbunda