Jumatatu , 25th Sep , 2017

Spika wa Bunge la Tanzania, Mh. Job Ndugai  amefunguka na kusema hafahamu kama Mbunge wa Jimbo la Ubungo, Saed Kubenea alikamatwa akiwa mgonjwa, anachojua alikamatwa kupelekwa kuhojiwa kwenye Kamati ya Maadili ambapo alikuwa tayari ameitwa.

Spika Ndugai amefunguka hayo wakati alipokuwa akifanya mahojiano na kipindi cha East Africa Breakfast cha East Africa Radio na kusema kwamba Kubenea alikuwa ameitwa na Kamati ya Maadili lakini yeye akawa ametoroka kurudi Dar es Salaam jambo ambalo lililazimu akamatwe na baada ya kufikishwa kwenye kamati akawa ameshindwa kuhojiwa kutokana na kuonekana kuwa hayuko sawa kiafya.

Spika Ndugai amesema Kamati kuendelea kukaa ofisini kwa muda mrefu ni gharama sana ndiyo maana polisi walitumika kumkamata na siyo walifanya kumkamata kwa sababu walikuwa wanajua kuwa ni mgonjwa.

"Hakukamatwa kwa sababu ni mgonjwa, Kubenea alitakiwa aonane na Kamati ya Maadili, yeye akatoroka kwenda Dar es salaam. Kamati kukaa hapa ndani ya wiki moja ni mishahara ya kutosha ndiyo maana polisi wakaenda kumkamata,  Kama alikamatwa akiwa mgonjwa ni bahati mbaya. "Hakukamatwa kwa sababu ni mgonjwa. Lakini kama ukiitwa kwenye mamlaka ya kimahakama lazima utoe ushirikiano kama unaumwa unasema tu na cheti cha daktari unaonyesha . Kama huumwi utakamatwa tu" amesema

Ameongeza kwamba "Kuwa mbunge hakukufanyi kuwa mtu mwenye mapembe. Lazima ufate sheria na taratibu zinavyotaka kwani mbunge ni sawa na mwananchi mwingine yeyote"

Katika hatua nyingine Spika Ndugai  amefunguka na kusema Mbunge anakuwa na kinga kidogo pale anapokuwa kwenye ukumbi wa bunge na akitoka nje anakuwa kama mwananchi wa kawaida na hata kinga yake inakuwa imepotea.

Ameongeza pia yeye kuagiza Wabunge kukamatwa wanaofanya vitu vya kutengenezea bunge picha mbaya ni kazi yake kwa sababu kiongozi huyo tayari amelihusisha bunge hivyo kuagizwa watu wanaotoa maoni yao mitandaoni wahojiwe ni sahihi.

"Mbunge anayeropokea popote mimi nitamshughulikia tu, kwani ni kudhalilisha bunge letu. Haijalishi kwamba umezungumzia ukiwa nchi gani au mtandaoni sisi lazima tukuhoji na wewe utakuwa umepata fursa nzuri ya kujieleza kuhusu nini ulikuwa unamaanisha" ameongeza.

Msikilize hapa chini Ndugai akifunguka