Jumapili , 24th Sep , 2017

Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Mohamed Bashe amefunguka na kuwataka watanzania kwa ujumla kuacha tabia ya ulalamikaji katika mambo yao wanayoyafanya bali wanapaswa kuweka juhudi ili waweze kufanya vizuri vitu vyao.

Mbunge wa Nzega Mjini Hussein Mohamed Bashe

Bashe ameeleza hayo kupitia ukurasa wake maalumu wa instagram asubuhi ya leo, huku nchi ikiwa imetanda wingu kubwa la baadhi ya watu kuilalamikia serikali kwa kila jambo wanalofanyiwa bila ya wao wenyewe kutambua kuwa wanatengenezewa misingi mizuri ya taifa lao la Tanzania. Baada ya serikali ya awamu ya tano kuanza kushughulikia vitendo vya rushwa katika sehemu mbalimbali za kutolea huduma pamoja na watu wanaokwepa kodi na kupelekea mzunguko wa pesa kwa baadhi ya watu kuwa mgumu, kwa kuwa walikuwa wanategemea njia za magendo kuendesha maisha yao.

"Sisi kama viongozi, wananchi na kama taifa, tusiwe walalamikaji tufanye juhudi katika kila jambo kulifanya vizuri. Juhudi huendana na jitihada na jitihada huanzia ndani ya nafsi na akili, na ili jitihada ichukue nafasi ni lazima tubadili 'attitude', hulka. Tukibadili tabia tutaacha kuwa watumwa wa 'historian' na tutaacha tabia ya kulaumiana na kuanza kuchukua hatua za kufanya juhudi", ameandika Bashe.