Jumanne , 26th Sep , 2017

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mwigulu Nchemba amewataka wananchi kuendelea kuwa na imani na vyombo vya ulinzi na usalama nchini katika kulinda raia na mali zao na hata watu wanaowafanyia uhalifu viongozi na wananchi watajulikana muda si mrefu.

Waziri Nchemba amesema kuwa watashughulika na mmoja mmoja hasa waliobeba jina la watu wasiojulikana, kwa hiyo wananchi waendelee kuliaamini jeshi la polisi nchini wakati huu ambapo wanaendelea na kazi ya upelelezi wa kuwa kamata watu wote waliohusika na mashambulio kwa Mbunge Tundu Lissu, Afisa mstaafu wa jeshi la wananchi na hakimu huko Mtwara kwani uchunguzi huo hauna ukomo mpaka wapatikane wote katika idadi yao waliohusika na mashambulizi.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Kinampanda Wilaya ya Iramba Mkoani Singida, ambapo amesema kuwa kama yeye ndiye aliyepewa dhamana ya usalama wa raia na mali zao katika Wizara ya Mambo ya Ndani basi hapata tokea hata kitongoji kimoja uchochoro ambao utaonekana umeshindikana ndani ya nchi.

"Kumetokea kasumba ya hawa watu wanaofanya maovu na kuitwa watu wasiojulika. Wanaofanya uhalifu wa aina hiyo dakika zao za kufika kwenye mkono wa sheria zinahesabika, vyombo vyetu hakuna sekunde hata moja wana lala. Taarifa inatolewa suala la uchunguzi linapokuwa limekamilika kwa asilimia zote. Si kwamba kwa kuwa hatujawahi kutangaza watu wakadhani kwamba hakuna kinachofanyika, liaminini jeshi lenu kwa sababu linashughulika na sisi kama serikali pamoja na  jeshi. Naahidi tutashughulika nao kweli kweli", Mwigulu amesema

Waziri Mwigulu pia ameongeza kwa kujibu kauli za watu mbali mbali wakiwepo viongozi wa upinzani wanaohitaji vyombo vya usalama kutoka nje ya nchi kufanya uchunguzi kwa ajili ya shambulio la Mbunge Tundu Lissu

"Nchi hii ni nchi huru inajitegemea, kuna watu wanasema wanataka vyombo vya nje vifanye uchunguzi, hawa watu wanamefanya uhalifu hapa  nchini, upelelezi utafanywa na watu wetu kwani hata hao wageni wakija nchini upelelezi watafanya kuuliza watu waliopo nchini. watakamatwa na vyombo vyetu na watafikishwa katika vyombo vya sheria vya hapa hapa  tunatakiwa kuamini vyombo vyetu, kama serikali tutashughulika kweli kweli na si kama hatujaanza kazi hiyo, hapa tunashughulika nao". ameongeza

Mtazame hapa chini Waziri akizungumza