Alhamisi , 19th Oct , 2017

Naibu Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mheshimiwa Kangi Lugola, amesema kasi ya kupambana na rushwa anayoenda nayo Rais Magufuli kwenye uongozi wake, wana CCM walijua atafanya hivyo kutokana na weledi wake.

Kangi Lugola ameyasema hayo leo alipokuwa akiongea kwenye kipindi cha East Africa Breakfast kinachorushwa na East Africa Radio, na kusema kwamba awamu zilizopita kulikuwa na mambo magumu ambayo yalishindikana kutatuliwa ikiwemo vitendo ya rushwa.

Pia Kangi amesema hata alipoingia madarakani Rais Magufuli watu hawakuwa na imani naye wakiamini ni kama wale waliopita, lakini imekuwa kinyume chake kwani sasa serikali haijahofia nguvu ya pesa ya watu hao, na kulifanyia kazi suala la rushwa bila uwoga.

“Yako mambo ambayo walikuwa wanadhani kwamba Rais Magufuli ni rais wa CCM kwa hiyo ni wale wale, lakini sisi tuliokuwa tunamjua kwamba tumepata chombo alipoingia madarakani, tulijua yale mambo magumu ambayo watu walikuwa wanatumia nguvu ya fedha, rushwa zilikuwa zimeshamiri hayawezekani, lakini rais wetu mambo yale magumu ameyafanyia kazi anasonga mbele na hakuna anachoogopa, ili mradi anayafanya kwa mujibu wa katiba”, amesema Kangi Lugola.

Kufuatia hayo Kangi Lugola ametangaza hali ya hatari kwa watu wanaotumia pesa kuvunja sheria ikiwemo kujenga viwanda maeneo ambayo hayaruhusiwi, kitendo ambacho kinachangia uharibifu wa mazingira.