Jumanne , 5th Apr , 2016

Jumla ya fedha za Tanzania shilingi trilioni nne nukta tano, zimekuwa zikikusanywa kila mwezi kupitia biashara ya kutuma na kupokea pesa kwa njia simu za mkononi inayotolewa na makampuni ya simu za mkononi nchini.

Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Mawasiliano nchini TCRA, Profesa Haji Semboja

Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Mawasiliano nchini TCRA, Profesa Haji Semboja, ametoa takwimu hizo jijini Dar es Salaam leo, mbele ya Kamati ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma, iliyokutana na watendaji wa TCRA kwa lengo la kupitia utendaji wa mamlaka hiyo.

Katika kikao na kamati hiyo, TCRA wameelezea majukumu kadhaa wanayoyatekeleza kama mamlaka ya udhibiti ambapo wamesema mamlaka hiyo haiendeshwi kwa mtazamo wa kibiashara bali kwa kusimamia usawa katika biashara na huduma ya mawasiliano nchini.

Kauli ya Profesa Semboja imekuja kufuatia michango mbali mbali ya wajumbe wa kamati hiyo, waliokuwa wakihoji utendaji wa TCRA ambapo pamoja na mambo mengine walitaka kufahamu sababu za upatikanaji na udhibiti wa huduma za mawasiliano nchini.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo wa bodi ya TCRA, Mamlaka hiyo mbali ya kusimamia sekta ya mawasiliano, lakini pia imekuwa ikifanya majukumu ya taasisi nyingine kama vile usimamizi wa kiasi cha biashara ya miamala ya pesa inayofanywa kupitia simu za mkononi kwa lengo la kuhakikisha mapato ya serikali hayapotei.