Jumapili , 17th Sep , 2017

Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu (CCM) ameomba watu waungane na kuweka tofauti za vyama au mitazamo tofauti ili kumwomba Mungu aweze kumponya mapema Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ambaye yupo jijini Nairobi kwa ajili ya matibabu

Mh. Nyalandu ambaye ambaye alifika hospitali kumjulia hali Mbunge Lissu amesema kwamba Mh. Lissu ameumizwa vibaya hivyo anaamini kwamba hatua zaidi na za haraka zitahitajika kumsaidia apate huduma za kitabibu katika ubora na ufanisi uliopo kwa sasa duniani.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Facebook Mh. Nyalandu ameandika, Ni maombi yangu kwetu sote , tuweke pembeni tofauti zetu za kiitikadi, ama mitazamo, tuungane na kushikamana kama Taifa kwa ajili ya kumwomba Mungu anyooshe mkono wake, na kumponya. Halikadhalika, sote tuungane kutoa msaada wa hali na mali kwa kadri ya uhitaji wake".

Mh. Nyalandu upade wa kushoto akiwa na mdogo wake Peter Nyalandu, katika hospitali ya The Nairobi Hospital, Kenya.

Aidha ameongeza , "Katika kuongea naye, Mh. Lissu ameonesha uso wa tabasamu, huku akimshukuru Mungu kwa kumruhusu kuwepo hai".

Hata hivyo imedaiwa kuwa Madaktari wanaendelea na hatua kadhaa za matibabu, wakiwa wameanza kwa kumuimarisha (stabilization), ili kuufanya mwili uweze kumudu hatua zaidi za utibabu anazopaswa kufanyiwa.