Thamani ya Lissu haielezeki- Mbowe

Monday , 11th Sep , 2017

Ikiwa zimepita siku kadhaa tokea lilipotokea tukio la kupigwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu na watu wasiojulikana, Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe amefunguka na kudai thamani ya Lissu ni kubwa kuliko kiwango chochote cha fedha.

Mbowe amebainisha hayo kupitia taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari na kuelezea mambo mengi kuhusiana na Lissu pamoja na likiwepo la gharama za matibabu ya kumtibia mwanasheria wao mkuu wa chama chao Mhe. Lissu.

"Mhe. Lissu ameumizwa sana, tena sana, ni ukweli usiopingika kuwa miujiza ya Mungu ni mikubwa hata kuweza kumuokoa katika bonde la mauti. Kutokana na ukweli huu, matibabu yake vilevile ni maalum na yanayohitaji wataalam wengi, vifaa tiba maalum na gharama kubwa. Hadi sasa zaidi ya shillingi millioni 100 zimeshatumika kuokoa maisha ya ndugu yetu Lissu", amesema Mbowe

Pamoja na hayo, Mbowe ameendelea kwa kusema "thamani ya Lissu, ni kubwa kuliko kiwango chochote cha fedha. Kila njia iliyo halali itatumika kupata fedha za kutosha kumtibu Mhe. Na hatimaye kumrudisha kwenye uwanja wa kudai haki, demokrasia na ustawi kwa wote nchini Tanzania", amesisitiza Mbowe.

Kwa upande mwingine, Mbowe amewashukuru watanzania kwa ujumla kwa namna wanavyoendelea kujitoa katika kumuombe Lissu huku akiwasisitizia wasiache kufanya hivyo.