Jumatatu , 8th Sep , 2014

Mamlaka ya mawasiliano nchini Tanzania TCRA imeonya kuwa itawachukulia hatua kali baadhi ya watu wanaotumia vibaya huduma za mawasiliano ya simu na mtandao wa intaneti, hasa wale wanaodhalilisha pamoja na kuhatarisha amani.

Msemaji wa Mamlaka ya Mawasiliano TCRA Bw. Innocent Mungy.

Mkurugenzi wa idara ya mawasiliano na elimu kwa umma wa TCRA Bw. Innocent Mungy, ametoa onyo hilo leo kufuatia kile alichosema kuwa ni kuongezeka kwa matukio ya watu kuvunja sheria kiasi cha kuhatarisha amani katika jamii.

Kwa mujibu wa Mungy, watu hao wachache wasio na maadili, wametumia vibaya maendeleo chanya ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano nchini, kwa kuweka picha zinazodhalilisha wenzao na zisizoendana na maadili ya Kitanzania.

Msemaji huyo wa TCRA amefafanua kuwa wasichana na mabinti wenye umri chini ya miaka 24 ndio wahanga wakubwa wa udhalilishaji katika mitandao ya kijamii kutokana na wengi wao kupigwa picha za utupu na kuwekwa katika mitandao ilhali wanaume wakiwa sio waathirika wakubwa.

Mungy ametahadharisha kuwa kuna uwezekano wa kutokea matukio ya uvunjifu wa amani katika jamii hasa baada ya kuibuka pia kwa makundi na kambi hasimu zinazogombana kupitia mitandao hiyo.

Amefafanua kuwa sheria ya mawasiliano ya simu na posta ya mwaka 2010 (EPOCA) inakataza watu kutumia vibaya huduma za mawasiliano na ambapo ametaja moja ya adhabu kwa wanaofanya hivyo kuwa ni kifungo cha miezi miezi mitatu jela na faini ya fedha za Tanzania shilingi laki Tano au adhabu zote kwa pamoja.