Jumanne , 23rd Mei , 2017

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amesema Tanzania imejiwekea malengo ya kuongeza uzalishaji wa umeme kutoka Megawatts kati ya 1,500 na 1,800 zinazozalishwa hivi sasa hadi kufikia Megawatts 10,000.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akiwa katika mazungumzo na Bw. Zhang Xin, Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya China National Machinery Industry Federation (CBMIF) na mjumbe wa National Congress ya China Bw. Zhang Xin aliyemtembelea Ikulu jijini Dar es salaam leo Machi 23, 2017

Rais Magufuli ameyasema hayo leo Ikulu Jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Makamu Mwenyekiti wa CNMIF na Mbunge wa Bunge la Wananchi wa China Bw. Zhan Xin na kuongeza kwamba ili kufikia malengo hayo wawekezaji wanakaribishwa kuzalisha umeme kwa kutumia vyanzo vilivyopo kama vile gesi, makaa ya mawe na jua.

Amewahakikishia wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Shirikisho la Taifa la Utengenezaji wa Mitambo ya Viwanda la China (China National Machinery Industry Federation - CNMIF) kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itawapa ushirikiano wa kutosha katika mpango wao wa kuwekeza katika uzalishaji wa nishati ya umeme, viwanda na kilimo hapa nchini.

“Kwa hiyo Ndg. Zhang Xin kawaambie wawekezaji wenzako wa China waje Tanzania, nchini zetu ni ndugu na marafiki wa miaka mingi, itakuwa jambo jema wakija kuunga mkono juhudi zetu za kujenga viwanda kwa kuzalisha umeme mwingi na pia kushiriki katika miradi mingine ikiwemo ya ujenzi wa miundombinu ya reli na barabara” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akizungumza na Balozi wa Ufaransa nchini Mhe. Malika Berak aliyemtembelea Ikulu jijini Dar es salaam leo Machi 23, 2017

Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amekutana na Balozi wa Ufaransa hapa nchini Mhe. Malika Berak ambapo viongozi hao wamezungumzia utekelezaji wa mambo mbalimbali ya ushirikiano pamoja na miradi ya maendeleo iliyotokana na makubaliano ya Mkutano wa wafanyabishara wa Tanzania na Ufaransa uliofanyika hivi karibuni.

Viongozi wengine ambao leo wamekutana na kufanya mazungumzo na Mhe. Rais Magufuli ni Kaimu Balozi wa Uturuki hapa nchini Bw. Yunus Belet na Kaimu Balozi wa Jamhuri ya Korea Bw. Songwon Shin.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akiwa katika picha na Kaimu Balozi wa Korea Kusini nchini Mhe. Songwon Shin, ofisa wa Ubalozi pamoja na Msaidizi wa Rais Maswala ya Diplomasia Bi. Zuhura Bundala aliyemtembelea Ikulu jijini Dar es salaam leo Machi 23, 2017