Jumanne , 22nd Aug , 2017

Waziri Mkuu Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye amesema kunyang'anywa mashamba yake si sababu ya yeye kufikiria kurudi CCM kwani wakati anaondoka na kuhamia CHADEMA aliamua kwa hiari yake mwenyewe kwa kuzingatia maslahi ya umma.

Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye

Akizungumza leo na Wanahabari, Mhe. Sumaye ambaye pia sasa ni Mwenyekiti wa CHADEMA kanda ya pwani amesema kwamba tangu kuondoka ndani ya Chama cha Mapinduzi amekuwa akiandamwa kwa na maneno pia na visa mbalimbali vya kumkatisha tamaa ya kuendelea kubaki upinzani lakini haiwezi kuwa rahisi yeye kubadilisha msimamo aliouweka.

“Kunyang’anywa mashamba yangu najua ni uamuzi wa juu haunidhoofishi nifikirie kurudi CCM. Suala la kufikiri kuninyang'anya mashamba itakuwa sababu ya kunirudisha CCM ni ndoto ya mchana, nilihama kwa maslahi ya wananchi na nilishasema mbele ya wanahabari kitakachonifanya nirudi CCM ni mpaka CCM itoke madarakani. lakini sina haja ya kurudi ,’’ Sumaye

"Wanataka nirudi CCM, mimi sitaki kurudi CCM, kwanini wananilazimisha? Nilisema sababu za kuondoka huko, waseme wazi sababu za kuyafuta mashamba yangu ni za kisiasa tu," aliongeza

Akizungumza kuhusiana na mashamba yake yaliyochukuliwa na Serikali, Mh. Sumaye amesema anashangaa kuambiwa kwamba mashamba yake hayalipiwi kodi wala kuendelezwa wakati shughuli nyingi zikiwemo ufugaji na kilimo zinafanyika ikiwa ni pamoja na umiliki wa kisheria.

Pamoja na hayo Sumaye amewataka viongozi waliopo madarakani kutotumia visasi vya kisiasa kumfilisi kwani chama cha upinzani kipo kisheria na pia siyo dhambi.