Jumatano , 13th Sep , 2017

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema amefunguka na kudai amesikitishwa na kitendo cha Spika wa Bunge, Job Ndugai kuwataka wabunge wawili kufika mbele ya Kamati ya Maadili na mwengine kamati ya ulinzi na usalama kuhojiwa juu ya kauli zao walizozitoa

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.

Mhe. Godbless Lema amesema hayo leo akiwa mjini Nairobi nchini Kenya alipokwenda kumjulia hali Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu ambaye ameshambuliwa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana. 

"Nimesikitishwa sana na kitendo cha Mhe. Spika kuwataka wabunge wawili, Mhe. Zitto Kabwe na Saed Kubenea kutokea  katika kamati ya maadili na mwingine kamati ya ulinzi na usalama na pengine baada ya maneno yangu haya na mimi naweza nikaitwa lakini siyo kitisho tena kwangu kuitwa mahali popote. Nipo Nairobi kumuangalia mbunge wetu na rafiki yangu, Mhe. Lissu ambaye hawezi kula wala kuinua mkono baada ya kupigwa na risasi na watu wasiojulikana", amesema Lema.

Pamoja na hayo, Lema ameendelea kwa kusema "Nilitarajia Mhe. Spika aliposikia taarifa za mbunge wake kupigwa risasi pengine shughuli za Bunge zote angesimamisha kama ambavyo alivyoamuru kukamatwa kwa wabunge wawili wapelekwe Polisi akiwemo Kubenea hapo awali", amesisitiza Lema.

Spika wa Bunge, Job Ndugai  

Kwa upande mwingine, Mhe. Godbless Lema amedai alitarajia kuona mabadiliko ya katika Bunge kwa kupitisha sheria kwa pamoja ili kusudi wabunge waweze kupatiwa ulinzi wa kutosha kuanzia majumbani kwao mpaka wao wenyewe lakini imekuwa tofauti na yeye alivyokuwa akifikiri.