Jumapili , 25th Jun , 2017

Jeshi la Polisi limewataka Waislam na Wananchi kusheherekea Sikukuu ya Eid El Fitr kwa utulivu na amani huku likiwahakikishia ulinzi na kuahidi kupambana na wale wote wataotaka kufanya uhalifu katika kipindi hiki cha sikukuu.

Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro

Akizungumza Mkoani Kilimanjaro, ambapo sherehe za Idd zinatarajiwa kufanyika kitaifa ambapo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa atakua Mgeni Rasmi, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro amesema jeshi hilo halitamvumilia mtu yoyote atakayefanya uhalifu katika msimu huu.

IGP Sirro amewataka waislam kuendeleza matendo mema waliyokuwa wakiyafanya katika kipindi chote cha Mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani ikiwemo kudumisha umoja, amani na ushirikiano.

Pamoja na hayo ameongeza kwamba, Sherehe hizo zinaunganisha taifa pamoja na dunia nzima kwa furaha na amani hivyo, Watanzania hawana budi kudumisha amani ya nchi iliyopo kwa sasa.