Alhamisi , 27th Jul , 2017

Walimu wa Shule ya Sekondari  ya Wasichana Jangwani wameishukuru kampuni ya East Africa Television LTD, Hawa Foundation pamoja na watanzania kupitia kampeni ya 'Namthamini' iliyowapatia wanafunzi taulo za kike kuwafanya wahudhurie masomo bila hofu.

Wanafunzi wa Jangwani Sec kwenye picha ya pamoja na watangazaji wa
EATV na EA radio wakionyesha zawadi za taulo za kike walizopokea kutoka watanzania kupitia kampeni ya 'Namthamini'

Akitoa shukrani leo wakati wa kupokea zawadi za taulo za kike kutoka kwa watanzania mbalimbali, Mwalimu Dokera wa wa shule ya Jangwani anayehusika na wanafunzi wenye ulemavu amesema kampeni ya 'Namthamini'  ni mkombozi kwa watoto wa kike na wanafunzi wasio na uwezo wa kununua taulo hizo.

"Wakati mwingine tunalazimika  kutoa fedha mifukoni mwetu  ili kuwanunulia wanafunzi wa kike taulo za kujihifadhi wakati wa siku zao. Haswa kwa hawa wanafunzi wenye ulemavu wanapata shida sana na wengi wao wanatoka mikoani. Kampeni ya 'Namthamini' ni faraja kwa wanafunzi hawa wa kike . Tunawashukuru watanzania waliojitoa kwa hali na mali na kuhakikisha wanawasaidia wanafunzi. Nawaomba wasiishie leo kwani bado mahitaji ni mengi kwa wanafunzi" alisema Mwalimu Dokera

  Mwalimu Dokera wa wa shule ya Jangwani anayehusika na wanafunzi wenye ulemavu

Hata hivyo ugawaji wa taulo za kike kwa shule za Dar es salaam ulifika mpaka shule ya Sekondari ya Wasichana Kisutu ambapo wanafunzi hao wameishukuru kampuni ya East Africa Television LTD na Hawa Foundation kwa kusema kwamba kampeni ya 'Namthamini' imewafikia kwa wakati muafaka ambapo wanafunzi wengi wa kike wamekuwa wakikabiliwa na changamoto wakati wa kupata siku zao kwani baadhi yao kukosa taulo za kujihifadhi.

 Mwanafunzi wa Kisutu Cleopatra Simon.

"Nasema asante kwa msaada huu ambao umetolewa na watanzania kwani tulikuwa tunapata changamoto kwa kushindwa kuhudhuria kwenye masomo hata siku tano ambapo ndani ya miezi sita ni mwezi mzima kitu ambacho kinadumaza ufaulu kwa watoto wa kike wengi hapa nchini"  Mwanafunzi wa Kisutu Cleopatra Simon.

Kwa upande wake Mratibu wa vipindi kutoka East Africa Radio Bi. Irine Tillya amesema kampeni hiyo ni mwendelezo wa kuhakikisha kwamba changamoto ya ukosefu wa taulo za kike kwa wanafunzi inamalizika.

Mratibu wa vipindi kutoka East Africa Radio na Mtangazaji wa East Africa Breakfast Bi. Irine Tillya akizungumza jambo na wanafunzi aliyeshikilia kipaza sauti

"Kampeni ya Namthamini ina lengo la kuwasaidi watoto wa ike kubaki shule na kusoma kwa uhuru wanapokuwa kwenye siku zao ndiyo maana East Africa Television LTD kwa kushirikiana na Hawa Foundation ilianzisha kampeni ya Namthamini mwezi wa tatu na kukusanya michango mbalimbali ambayo leo tumewafikishia nyinyi," Irene Tillya 

Mtangazaji wa 'Hot Mix akikabidhi  taulo za kike kwa Mwalimu mkuu msaidizi wa Kisutu