Jumatatu , 28th Sep , 2020

Mgombea wa Urais kwa tiketi ya Chama cha ADA TADEA, John Shibuda amezindua rasmi kampeni zake za urais huku akiahaidi kupambana na mambo matatu ambayo ni umaskini, ujinga na maradhi ili kuhakikisha utawala bora.

Mgombea wa Urais kwa tiketi ya Chama cha ADA TADEA, John Shibuda

Akizungumza na wananchi wa wilaya ya Maswa, Mkoani Simiyu kwenye uzinduzi wa kampeni zake Shibuda ,ameweka wazi kuwa hawana tataizo na vyama vingine vya siasa nchini.

“Sisi kama Chama cha ADA TADEA hatuna tatizo lolote na vyama vingine vya siasa bali tatizo letu kubwa ni mapambano dhidi ya madhira matatu ambayo ni; ujinga, maradhi na umaskini, na vita ya chama chetu ni kuhakikisha kuwa utawala bora unapatikana” alisema Shibuda

Aidha Shibuda amesema kuwa  endapo chama hicho kitapewa ridhaa na watanzania kimejipanga kuhakikisha kinaondoa maadui wakubwa wa ustawi na maendeleo ya jamii nchi huku akiwasisitiza  watanzania kumpigia kura za ndio katika nafasi ya urais.

Chama cha ADA TADEA kimezindua rasmi kampeni zake kitaifa mkoani Simiyu wilayani Maswa tarehe 27/09/2020 na kimetaja utawala wa sheria na siasa safi kuwa moja ya vipaumbele vyake.