Jumatatu , 25th Jan , 2021

Serikali imeyaonya makampuni ya simu ambayo watumishi wao wamekuwa sio waaminifu na wamekuwa wakivujisha siri za wateja wao kwa watu wengine na kuwataka wananchi wenye malalamiko kama hayo kuyawasilisha wizarani ili hatua kali za kisheria zichukuliwe.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt Faustine Ndugulile

Hayo yamebainishwa Jijini Dodoma na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt Faustine Ndugulile wakati wa hafla ya kutiliana saini mikataba kati ya Makampuni ya simu na Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF) ili kupeleka mawasiliano maeneo ya vijijini ambapo amesema  kuna makampuni ya simu ambayo watumishi wao si waaminifu na wamekuwa wakivujisha siri za wateja kwa marafiki zao kwa kuhongwa fedha.

"Kumekuwa na tabia kwenye haya makampuni watumishi wanavujisha siri za mawasiliano za wateja mtu kagombana na mpenzi wake anakuja kwenu mnamkopia mawasiliano yake yote hilo halikubariki" amesema Dkt Ndugulile.

Aidha ameyataka Makampuni hayo kukomesha tabia hiyo sambamba na  kuanza kuangalia namna ya kuboresha huduma zao kwa kuondoa huduma ya interneti ya kasi ya 2G na ili kama nchi tuanzie kasi ya 3G na kuendelea mbele kama nchi nyingine huku akihimiza kupunguza gharama za bando kwa wateja wao.