Jumanne , 17th Jan , 2017

Serikali imesitisha agizo lake lililokuwa linawataka wenyeviti wa Serikali za Mitaa kote nchini kurudisha mihuri katika Halmashauri za Wilaya na kuwapatia Watendaji wa Mtaa kuitumia mihuri hiyo katika shughuli mbalimbali za utendaji katika ngazi hiyo

George Simbachawene - Waziri wa TAMISEMI

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam Waziri wa nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. George Simbachawene, amewataka wenyeviti wa serikali za mitaa waendelee kutumia mihuri hiyo kama ilivyokuwa hapo awali mpaka pale utaratibu mwingine utakapotangazwa na kwamba uamuzi huo utawashirikisha ili kuleta ufumbuzi wa matumizi ya mihurio hiyo.

Mhe. Simbachawene amesema, hapo awali serikali ilikuja na uamuzi huo kama suluhisho la kuondokana na tabia ya wenyeviti wa serikali za mitaa wasio waadilifu ambao wanatumia mihuri hiyo vibaya kwa kuuza mali na mashamba ya kijiji, na wakati mwingine kupelekea migogoro mikubwa ya ardhi hapa nchini ikiwemo ya wakulima na wafugaji, na kutoa ardhi kwa wawekezaji kinyume cha sheria.

Aidha, Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Halmashauri ya Ubungo na Kinondoni ambaye ni Mwenyekiti wa Mtaa wa Mwongozo Bw. James Ngoitanile amewataka wenyeviti wa serikali za mitaa kote nchini kutofurahia kurudishiwa mihuri hiyo na badala yake wapime utendaji wao na kuondoa kasoro zote zinazolalamikiwa.