Jumatatu , 16th Jan , 2017

Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imepanga kukutana na wadau wa habari nchini ili kujadili mapungufu yaliyopo kwenye sheria ya huduma ya habari nchini lengo likiwa ni kuongeza ufanisi katika utendaji wa vyombo vya habari.

Nape Nnauye

Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye, kwenye mahojiano na East Africa Television (EATV), ilipotaka kujua jitihada gani zinazofanywa na serikali za kuhakikisha vyombo vya habari nchini vinafanya kazi zake kwa uhuru na uwazi.

Mhe. Nnauye amesema kuwa wameamua kukutana na kuwashirikisha wadau wa habari ili kujua sheria hiyo inasaidiaje na ina mapungufu gani katika kutekeleza majukumu yao ili ifanyiwe marekebisho na kuleta ufanisi kwa tasnia ya habari nchini.

Katika hatua nyingine Waziri Nnauye amewataka wasimamizi wa vyombo vya habari nchini wahakikishe wanachunguza namna vipindi vinavyorushwa kwa kuzingatia maadili na taaluma ya habari ili kuepuka adhabu ambazo zinaweza kuleta hasara kwa chombo husika.