Ijumaa , 22nd Jan , 2021

Halmashauri ya wilaya ya Geita, imetenga bajeti ya shilingi bilioni 78, kwa mwaka wa fedha 2021/2022, huku ikija na mpango wa kugawa saruji kila Kata, ambazo zitatumika katika uanzishaji wa ujenzi wa vyumba vya madarasa na zahanati.

Saruji

Hayo yamejiri hii leo Januari 22, 2021, mara baada ya baraza la madiwani wilayani humo, kumaliza kupitisha mpango wa bajeti kwenye baraza hilo, huku baadhi ya madiwani hao akiwemo Jeremia Ikangala, akisema kuwa mpango wa kupeleka saruji katika kila Kata za wilaya hiyo utapunguza changamoto ya miundombinu ya shule katika kata zao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM wilayani humo Barnabas Mapande, amewahamasisha wazazi kujitahidi kupata vyeti vya kuzaliwa vya watoto wao ili kupunguza usumbufu wakati wa usajili ngazi mbalimbali ya elimu.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Donald Nsoko,amesema kuwa wanakabiliwa na upungufu wa vyumba vya madarasa hivyo wametenga zaidi ya shilingi milioni 94, kwa ajili ya uanzishai na umaliziaji wa ujenzi wa vyumba vya madarasa.