Alhamisi , 26th Mei , 2022

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amewakaribisha wawekezaji kutoka Canada kuja nchini kwa ajili ya kuwekeza katika viwanda vya utengenezaji wa simu janja hapa nchini. 

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye.

Nape amesema hayo hii leo Mei 26, 2022, jijini Dar es Salaam, katika kikao cha kubadilishana uzoefu na Katibu wa Mambo ya Nje wa Canada, Robert Oliphant, ambapo walijadili masuala mbalimbali ya habari na teknolojia ya habari. 

"Eneo ambalo tulitamani kama serikali kupata wawekezaji, ni eneo la upatikanaji  wa simu janja (smart phones na tablets), ili  ziwe na bei nafuu na watu waweze kumudu kununua," amesema Waziri Nape. 

Aidha Waziri Nape ameongeza kuwa, kutokana na Tanzania kutokuwa na viwanda vya kutengeneza simu janja imesababisha vifaa hivyo kuwa na gharama ya juu, hivyo kupelekea idadi chache ya Watanzania kuweza kumiliki simu hizo ambapo ni asilimia 27  tu ya Watanzania ndio wanaomiliki simu janja na asilimia inayobaki wanamiliki simu za kawaida, 

"Sasa imefika wakati simu janja zizalishwe hapa nchini, ili bei iwe ya chini na kila Mtanzania aweze kupata kifaa hicho, na hata huduma ikiboreshwa ina maana watu wengi watapata hiyo huduma," ameongeza