Jumamosi , 10th Dec , 2016

Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli amepewa siri ya kuendelea kuwa imara kimwili hata kama atafikisha umri mkubwa kuwa ni lazima aoe wake wawili.

Rais Magufuli akihutubia katika sherehe za uhuru

Ushauri huo amepewa na Rais wa Awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Alhaj Ali Hassan Mwinyi, ambaye amefanikiwa kudumu na uimara wake licha ya kuwa na umri mkubwa kiasi cha kuendelea kuhudhuria sherehe mbalimbali za kitaifa pamoja na mialiko mbalimbali.

Rais Magufuli ndiye aliyetoboa siri hiyo jana katika hotuba yake wakati akitoa salamu za maadhimisho ya siku ya uhuru wa Tanzania Bara, katika sherehe zilizofanyika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Wakati akiwashukuru na kuwapongeza viongozi wakuu wa nchi waliomtangulia kwa kazi nzuri walizofanya, Rais Magufuli alimtaja Mzee Mwinyi kama mtu wa mafano katika kutunza afya yake na kwamba hata yeye alimuomba ushauri wa kitu cha kufanya ili awe kama yeye kipindi atakapozeeka.

Rais Magufuli akimsalimia Mzee Mwinyi katika sherehe za Uhuru.

 

Rais Magufuli alisema kuwa ushauri aliopewa na Mzee mwinyi ni pamoja na sharti la kuwa na wake wawili.

"Hata mimi nilipomuomba ushauri anipe siri ya kuendelea kuwa kijana hadi leo lakini akaniambia sharti la kwanza ni lazime niwe na wake wawili" Alisema Rais Magufuli.

Inawezekana Rais Magufuli aliibua suala hilo kama utani kutokana na ukweli kwamba Mzee Mwinyi mwenye umri wa miaka 91 ana wake wawili wakati Rais Magufuli ambaye ana umri wa miaka 57 ana mke mmoja kwa sasa.

Mzee Mwinyi alikuwa Rais wa Tanzania kati ya mwaka 1985 na 1995.