Jumatatu , 20th Nov , 2017

Kiongozi wa muungano wa upinzani (NASA) nchini Kenya, Raila Odinga amezungumzia uamuzi uliotolewa na mahakama ya juu wa kuidhinisha uchaguzi wa Uhuru Kenyatta na kudai kwamba uamuzi huo umefanywa kwa shinikizo na kwamba wao hawatambui ushindi huo.

Taarifa iliyotolewa na mshauri wake Salim Lone, amesema kuwa serikali ya Jubilee sio halali na kuongeza kwamba  uamuzi huo wa mahakama ya juu ulifanywa kupitia shinikizo.

''Sisi watu wa Nasa tayari, tulikuwa tumeamua kabla ya uamuzi wa mahakama kwamba hatuitambui serikali ya Uhuru Kenyatta. Uamuzi huo haujabadilishwa na uamuzi wa mahakama ya juu ambao haukutushangaza. Ni uamuzi uliotolewa chini ya shinikizo kubwa, hatushutumu mahakama tunaihurumia''. Lone.

Aidha Lone amedai kwamba mahakama ilikutana chini ya shinikizo kubwa, baada ya kushindwa kukutana kutokana na wasiwasi mkubwa wa kiusalama kufuatia kupigwa risasi na kujeruhiwa kwa dereva wa naibu jaji mkuu kabla ya kusikizwa kwa kesi ya uchaguzi wa tarehe 26 Oktoba.

Mahakama ya juu leo imeidhinisha ushindi wa Kenyatta kutokana na kura zilizopigwa Oktoba 26. Uchaguzi wa kwanza uliofanyika Agosti 8 ulifutwa na mahakama hiyo kutokana na kudaiwa kuwa batili na siyo halali.