Jumanne , 27th Sep , 2016

Shirika la Ndege la Precision Air, limerudisha rasmi safari zake za kuelekea HAHAYA nchini Comoro kuanzia leo tarehe 27 Septemba 2016.

Ndege ya Precision Air

Akizungumzia kurejeshwa kwa safari hizo Mkurugenzi wa biashara wa shirika hilo Robert Owusu amesema kuwa Precision Air imejipanga kutoa huduma ya uhakika ya usafiri wa anga kati ya Tanzania na Comoro, ambayo itarahisisha biashara na safari kati ya nchi hizo.

“Safari zetu zitakuwa kila siku ya Jumanne, Alhamisi na Jumamosi kwa ratiba ambayo imepangwa mahususi kukidhi mahitaji ya safari za kiserikali, kibiashara na hata zile za mapumziko na kulingana na mapokeo ya soko tunatarajia kuongeza safari zaidi.” Amesema Owusu.

Pia amedokeza “Tuna furaha kurudisha safari hizi kama tulivyo ahidi , na hii itakuwa sehemu ya 13 katika mtandao wetu kwa ujumla na ni ya pili kwa safari zetu za kikanda".

"Nimatazamio yetu kutengeneza mtandao wa safari ambao utawawezesha abiria wetu kuunganisha safari zao ndani ya Afrika Mashariki, Afrika na Duniani kwa ujumla. Tunajivunia kuwa na mtandao bora zaidi unaowapa wateja urahisi wa kuunganisha safari zao na hatutachoka kuuboresha kuhakikisha tunaendana na matakwa ya soko.” Amesisitiza Owusu.

Precision air ndilo shirika pekee la Kitanzania lililo chini ya umoja wa Mashirika ya Ndege Duniani IATA na hivyo huwawezesha abiria kufanya 'booking' zao na kuunganisha na mashirika mengine ya Kimataifa.

Aidha kwa safari za ndani Precision Air inasafiri kwenda sehemu 13 ikitokea Dar es Salaam kuelekea Arusha, Kilimanjaro, Mwanza, Bukoba, Musoma, Tabora, Kigoma, Mtwara, Zanzibar and Pemba.

Ndege kuelekea Comoro iliondoka saa 4 asubuhi na ilitarajiwa kuwasili huko saa 5 asubuhi.

Awali Precision Air ilisitisha safari hizo mnamo mwaka 2014 na kutangaza kuzirejesha mapema mwezi Agosti mwaka huu.