Jumatano , 22nd Nov , 2017

Utafiti wa shirika lisilo la kiserikali la Twaweza umebaini kuwa Idara za Polisi na Mahakama bado zinaongoza kwa rushwa, licha ya kuwa ni taasisi zinazohudumia idadi kubwa ya watu.

Hayo yamebainishwa kwenye uzinduzi wa ripoti ya utafiti huo iliyopewa jina "Hawashikiki" uliofanyika leo jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wadau kutoka sekta za umma na kibinafsi.

Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti huo, wananchi wanaripoti kuwa licha ya viwango vya rushwa kupungua nchini kwa mwaka huu, bado idara za polisi na mahakama zimeendelea kuwa na kiwango kikubwa cha rushwa ambapo kati ya 36% na 39% ya wananchi waliohojiwa, wameiambia Twaweza kuwa waliombwa rushwa mara ya mwisho walipofika katika taasisi hizo.

Hata hivyo Mkurugenzi wa Utetezi wa Twaweza Bi. , Anastazia Lugaba, amesema kuwa wananchi walitoa rushwa ili kupata huduma ya uhakika katika sekta hizo lakini kwa sauti za wananchi zinazoonesha matumaini katika mapambano dhidi ya rushwa.

Ndani ya utafiti huo pia wananchi wamezungumzia sakata maarufu la kampuni ya madini ya Acacia wakiliweka katika kundi la rushwa kutumika kwa kiasi kikubwa, huku Mamlaka ya Mapato ya Tanzania pamoja na Mamlaka ya Bandari nazo zinaonekana kushughulikiwa ipasavyo na Taasisi ya Kuuzuia na Kupambana na Rushwa Takukuru huku wakitaja vyama vya upinzani vingelifanya vizuri zaidi katika kupambana na rushwa endapo vingepata nafasi ya kuwa madarakani .