Jumanne , 10th Oct , 2017

Mgombea Urais kupitia muunganiko wa vyama vya upinzani nchini Kenya, Raila Amolo Odinga, amejiondoa kwenye kinyang'anyiro hicho, baada ya viongozi wa Tume ya Uchaguzi Kenya IEBC, kukataa kuachia madaraka.

Akiongea na vyombo vya habari jijini Nairobi Kenya, kiongozi huyo wa upinzani ameituhumu Tume inayosimamia uchaguzi nchini humo IEBC kwa kutotaka kubadili uongozi wake, ambao wanaamini unampendelea Uhuru Kenyatta.

“Kwenye katiba ya demokrasia, hatukutakiwa kubishana kuhusu uchaguzi huru na haki, tulitakiwa kufanya kazi kwa pamoja kuhakikisha tunasimamia uchaguzi huu na mfumo wake wa kielektoniki, lakini kuendelea na uchaguzi bila marekebisho kwenye IEBC ni misingi ya vikwazo kwa huu uchaguzi, uchaguzi pekee ambao Jubilee wanataka ni ule ambao lazima watashinda hata kama sio kwa sheria”, amesema Raila Odinga.

Uamuzi huo wa Raila Odinga umekuja siku moja baada ya Uhuru Kenyatta kumtaka ajitoe kwenye kinyang'anyiro kama hayuko tayari kurudia uchaguzi huo ulioamriwa na mahakama.

Pamoja na hayo viongozi hao wa NASA wameitisha maandamano ya nchi nzima hapo kesho asubuhi, ili kupinga kitendo cha Tume ya Uchaguzi kutobadili uongozi wake.

Septemba 1, 2017 Mahakama ya Juu nchini Kenya ilfuta matokeo ya uchaguzi wa Urais baada ya NASA kuishtaki IEBC kwamba walifanya udanganyifu na kukutwa na hatia, na kuamuru uchaguzi huo urudiwe ndani ya siku 60, ndipo Tume ya Uchaguzi ikaitangaza Oktoba 26 kuwa siku ya uchaguzi wa Urais.
 

 

 

 

Endelea kubaki nasi kwa taarifa zaidi.