Ijumaa , 30th Oct , 2020

Nyumba ya Mbunge mteule wa Jimbo la Shinyanga Patrobas Katambi wa Chama cha mapinduzi CCM imenusurika kuchomwa moto usiku wa kuamkia leo na watu wasiojulikana.

Mbunge mteule wa jimbo la Shinyanga Mjini Patrobas Katambi

Kamanda wa jeshi la polisi Mkoani Shinyanga, Debora Magiligimba, amesema tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia leo majira ya saa sita 6: 45 usiku katika mtaa wa Ushirika Manispaa ya Shinyanga, ambapo Patrobas Katambi akiwa amelala nyumbani kwake pamoja na ndugu zake alisikia kishindo juu ya paa la choo cha nje na walipoangalia waliona moto unawaka nakuanza kuuzima moto huo.

Aidha baada ya kufuatilia waliona gari aina ya Toyota Clugger lenye rangi ya Silver limepaki pembeni huku watu wawili wakikimbia kwenda kupanda gari hilo.

Kamanda Magiligimba amesema kuwa baada ya kufuatilia gari hilo wamebaini kuwa ni la aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo la Shinyanga mjini Salome Makamba kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambaye anatafutwa na jeshi la polisi pamoja na mdogo wake Timoth Makamba.

Tayari watu wawili wamekamatwa na jeshi la polisi ambao ni Wilson Saluti, na Jackson Peter, wakiwa ndani ya gari hilo lenye namba za usajili T 729 DFP mali ya Salome Makamba.