Jumatano , 20th Sep , 2017

Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu amedai amekuwa akisubiri ripoti ya madaktari wa Nariobi ili kumruhusu Mbunge Tundu Lissu waweze kumpeleka katika hospitali ya madaktari bingwa wa Marekani, lakini bado wamekuwa wazito kuwaandikia ripoti.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Mh. Nyalandu ameandika kwamba alirudi jijini Nairobi kwa ajili ya maandalizi ya uwezekano wa kumhamishia Mh Lissu Marekani kwa ajili ya huduma yenye ubora zaidi, endapo madaktari wa Nairobi wangeridhia.

"Tumekuwa Nairobi Hospital tukisubiri madaktari watoe ripoti ya mwenendo wa matibabu ya Mh Tundu Lissu kwa minajili ya kuwapatia madaktari bingwa wa Marekani na kuona uwezekano wa Mh Tundu Lissu kupatiwa rufaa kwa matibabu zaidi nje, lakini bado kalamu zao ni nzito kuandika ripoti hii siku ya tatu tangu tuahidiwe"

Ameongeza kuwa "Kesho asubuhi (leo) itarejea hospitalini kusikiliza kauli ya mwisho yamadaktari  kuhusu ripoti hiyo".

Mbunge Tundu Lissu alipelekwa hospitali ya Nairobi kupatiwa matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana alipokuwa ametoka kwenye vikao vya bunge majira ya mchana maeneo ya Area D mkoani Dodoma.

Taarifa kutoka kwa viongozi mbalimbali waliomtembelea hospitalini hapo wamekuwa wakitoa shuhuda kuwa Mbunge Lissu alijeruhiwa na anahitaji matibabu yaliyo bora zaidi ili kuokoa maisha yake.