Jumanne , 23rd Mei , 2017

Wanawake nane kati ya 10 wenye ugonjwa wa fistula wanaopokelewa katika hospitali ya walemavu ya CCBRT Jijini Dar es Salaam huwa wanafanyiwa vitendo vya unyanyapaa kwenye ngazi ya familia na jamii kutokana na kuugua ugonjwa huo.

Msimamizi mkuu wa wodi ya wagonjwa wa fistula katika hospital ya CCBRT, Bi. Mariam Karata ameaimbia Kurasa ya EATV kuwa katika wanawake hao kumi, saba kati yao nao wamechwa na waume zao baada ya kupata maradhi hayo ya Fistula.

Kwa upande wao baadhi ya wanawake waliopata ugonjwa huo wameziomba familia na jamii kuacha kuwanyanyapaa watu wenye tatizo la Fistula badala yake kuwasaidia kwa kuwapa elimu ambayo itawasaidia kupata matibabu sahihi kwa kuwa ugonjwa huo unatibika kabisa.

"Sisi tuishauri jamii, Fistula ni tatizo...Tunaita fistula ya uzazi kwa sababu inawapa wakina mama kipindi cha kujifungua kutokana na uchungu pingamizi wa muda mrefu na fistula inatibika wasiwanyanyapae.....Hili tatizo linaweza likamkuta mtu yoyote hakuna anayemjua litakayemkuta lakini ni tatizo ambalo halitokani na imani za kishirikina". Alisema Karata 

Takwimu za ugonjwa wa fistula hapa nchini zinaonesha kuwa takribani wanawake elfu 3 wanapata tatizo la ugonjwa huo kila mwaka kati ya hao nusu yake ndio wanafika hospitali kwa ajili ya kupata matibabu.