Jumatano , 18th Jan , 2017

Jaji Mkuu Mstaafu Mohamedi Othman Chande amezitaka mahakama kufanya kazi kwa kuendana na kasi ya awamu ya tano pamoja na kufuata maadili ya taaluma ya sheria katika kutoa haki na sawa kwa wakati na kwa watanzania wote.

Jaji Mkuu Mstaafu - Mohamed Chande Othman

 

Jaji Chande ameyasema hayo mara baada ya kuapishwa kwa Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania Prof Ibrahim Hamis Juma ambapo amesema kuwa kuongezeka kwa uwazi katika shughuli za mahakama kutasaidia sana katika kuendeshwa kwa kesi na kuamuliwa kwa wakati na watendaji wake.

Amesema anafurahi anauacha muhimili wa mahakama katika hali nzuri huku akiwataka watendaji kuendeleza juhudi za kuboresha mifumo taratibu na sheria ili kutoa nafasi zaidi kwa kesi nyingi kushughulikiwa kwa haraka ikiwemo usikilizwaji wa kesi.

Akizungumzia kuhusu mpango wa maendeleo wa miaka mitano ambao ameuacha amesema kuendelezwa kwa mpango huo kutasaidia kuharakisha usikilizaji wa kesi, kuongeza mfumo wa usikilizwaji wa kesi pamoja na ushirikiano na ofisi ya mwanasheria mkuu, mkurugenzi wa mashikata pamoja na polisi ikiwemo uboreshaji wa njia ya kuwahudumia wateja wengi zaidi.

Rais Magufuli na majaji wa Mahakama ya Rufaa mara baada ya kumuapisha Kaimu Jaji Mkuu

Akieleza kwa upande wa mahakama ya mafisadi amesema kuwa mahakama hiyo ni ya juu na kuwa suala la rushwa na ufisadi zinashughulikiwa katika ngazi hiyo licha ya kuwepo kwa utaratibu wa kusikilizwa kwa kesi ambazo tayari zimekamilika kwa upande wa upelelezi pamoja na ushahidi ili kurahisisha kumaliza kesi kwa wakati.

“Tumepokea maombi matatu ambayo ni ya dhamana lakini nadhani mwaka huu hasa kesi zinaweza zikaanza katika kanda 13 za mahakama kuu” alisema Jaji Chande

Rais Magufuli akimuapisha Kaimu Jaji Mkuu