Jumatano , 21st Jun , 2017

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa familia, wanachama wa CCM, uongozi wa Yanga na wana michezo kiujumla kufuatia kifo cha shabiki wao mkubwa Ali Mohamed, maarufu kama Ally Yanga.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli

Ali Yanga amefariki jana tarehe 20 Juni, 2017 kwa ajali ya gari iliyotokea katika Kijiji cha Chipogolo kilichopo katika Wilaya ya Mpwapwa Mkoani Dodoma.

Katika Salamu za Rais Magufuli amesema  atamkumbuka Ali Yanga kwa uzalendo wake na mchango wake wa kuhamasisha na kushabikia masuala mbalimbali ya kitaifa na hasa michezo, ikiwemo kuishabikia timu yake ya Yanga, timu ya soka ya taifa, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na shughuli za kiserikali kama vile Mwenge wa Uhuru na ziara za viongozi.

Nimeguswa sana na kifo cha Ali Yanga, nilikuwa naye wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ambapo alitoa mchango mkubwa katika uhamasishaji wa wananchi kukipigia kura chama changu cha CCM, na pia amekuwa akiongoza mashabiki wenzake kuishabikia timu ya Yanga na timu ya taifa bila kuchoka, kwa kweli alikuwa hodari sana katika ushabiki wake" alisema Rais Magufuli

                       Marehemu Ally Mohamed maarufu kama Ally Yanga

Pamoja na hayo Rais ameendelea kwa kusema “Natoa pole nyingi sana kwa familia yake, viongozi wa timu ya Yanga, wanamichezo wote, wana CCM na wote walioguswa na kifo cha Ali Yanga na namuombea kwa Mwenyezi Mungu aipumzishe roho yake mahali pema peponi, Amina”