Jumatatu , 16th Jan , 2017

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezindua safari za ndege za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kutoka jijini Dar es Salaam kwenda Makao Makuu ya Nchi, Dodoma.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea mfano wa Boarding Pass kutoka kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mahandisi Edwin Ngonyani kabla ya kusafiri kwa ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kutoka uwanja wa ndege wa Julius Kambarage Nyerere, Dar es salaam kwenda Dodoma Januari 16, 2017. Alikuwa akizindua safari za ndege za shirika hilo kati ya viwanja viwili hivyo.

Akizindua safari hizo leo amesema safari hizo zitawezesha wafanyabiashara na wananchi wengine kutoka Dodoma na kwenda katika maeneo mengine kwa urahisi.

“Tuna ndege nzuri. Tuzitumie kwenda katika maeneo mengine kwani gharama zake ni nafuu. Kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam ni sh. 165,000, kwenda na kurudi ni  sh. 299,000,” amesema.

Amesema ndege nyingine kama hiyo inatarajia kuwasili nchini Juni mwaka huu jambo ambalo litaongeza idadi ya safari za ndege hizo nchini na maeneo mengine ya nchi jirani.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia viongozi na wananchi wa Dodoma baada ya kutua kwenye uwanja wa ndege wa Dodoma akitoka uwanja wa ndege wa Julius Kambarage Nyerere jijini Dar es salaam Januari 16, 2017 ikiwa ni uzinduzi wa Safari za ndege za Shirika hilo kati ya viwanja viwili hivi. 

Kwa upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa ATCL. Kapten Richard Shaidi ametumia fursa hiyo kuipongeza Serikali kwa ujio wa ndege hizo na kwamba hiyo ni moja ya mikakati ya Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli ya kufufua ATCL.

“Hivi karibuni tunaanza kwenda nchi jirani. Mwakani tutapata ndege nyingine kubwa itakajayokuwa inafanya safari za masafa ya kati na ya mbali” amesema.

Aidha, Mwenyekiti wa Bodi ya ATCL, Bw. Emmanuel Korosso amesema hivi karibuni shirika hilo linatarajia kuanza safari za kwenda katika miji ya Tabora, Songea, Mtwara, Mpanda, Mafia na Jiji la Tanga.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisafiri kwa ndege ya Bombardier Q400 ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kutoka uwanja wa ndege wa Julius Kambarage Nyerere kwenda Dodoma Januari 16, 2017. Alikuwa akizindua safari za ndege za ATCL katika viwanja viwili hivyo. Kushoto kwake ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Leonard Chamuriho.

Akizungumzia kuhusu safari za Dodoma amesema zitafanyika mara mbili kwa wiki, siku ya Ijumaa na Jumatatu. Hata hivyo wanatarajia kuongeza safari hapo baadae.

Naye Spika wa Bunge, Mheshimiwa Job Ndugai ametoa wito kwa wakazi wa Dodoma kutumia vizuri fursa hiyo ya safari za ndege za ATCL kwa kuwa utawawezesha kusafiri kwa muda mfupi tofauti na vyombo vingine vya usafiri.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Bw. Jordan Rugimbana ameshukuru kwa uanzishwaji wa safari hizo kwa kuwa zitarahisisha kutoka katika Makao Makuu ya nchi na kwenda katika mikoa mingine nchini.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Waziri Mkuu Mstaafu, John Malecela baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa Dodoma akitoka uwanja wa ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam ikiwa ni uzinduzi wa safari za ndege za ATCL kati aya viwanja viwili hivyo, Januari 16, 2017.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Spika wa Bunge, Job Ndugai baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa Dodoma akitoka uwanja wa ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam ikiwa ni uzinduzi wa safari za ndege za ATCL kati aya viwanja viwili hivyo, Januari 16, 2017.