Mwili wa mtekaji Arusha bado mtihani

Tuesday , 12th Sep , 2017

Baada ya kuwepo taarifa  za familia ya marehemu Samson Peter kugoma kuzika mwili wa kijana huyo ambaye aliwateka na kuwaua watoto wawili, hospitali ya Mt. Meru imesema haijapokea taarifa zozote kuthibitisha hilo na kwamba mwili huo bado wameuhifadhi.

Samson Peter

Habari zilizopo kutoka kwa msimamizi wa chumba cha kuhifadhia maiti Hospitalini hapo, Francis Coster akiongea na kituo kimoja cha TV amesema hakuna ndugu yeyote aliyejitokeza kuja kudai mwili kwaajili ya maziko na wamekuwa wakisikia taarifa za kugomewa mwili huo kutoka kwenye vyombo  vya habari.

Aidha amebainisha kuwa taratibu za maziko ya marehemu  mbalimbali ambao  ndugu zao hawakujitokeza mapema hospitali hufanya taratibu za mazishi  baada ya siku 21.

Samsoni alifikwa na mauti kwa kupigwa risasi na Polisi  Murieti Jijini Arusha September 6, mwaka huu alipojaribu kutoroka wakati akienda kuwaonyesha askari watu alioshirikiana nao kufanya utekaji na mauaji hayo.