Ijumaa , 24th Mar , 2017

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, amewaapisha Mawaziri wawili, Katibu Mkuu Ikulu, Mabalozi wanne na Kamishna wa Tume ya Mahakama, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Viongozi walioapishwa leo wakila kiapo cha maadili ya utumishi wa umma, Ikulu DSM

Walioapishwa ni Mhe. Dkt. Harrison George Mwakyembe aliyeapishwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Prof. Palamagamba Aidan John Mwaluko Kabudi aliyeapishwa kuwa Waziri wa Mambo ya Katiba na Sheria, na Bw. Alphayo Kidata aliyeapishwa kuwa Katibu Mkuu – Ikulu.

Wengine ni Mhe. Sylvester Mabumba aliyeapishwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Comoro, Mhe. Dkt. Abdallah Possi aliyeapishwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Mhe. Job Masima aliyeapishwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Israel na Mhe. Jaji Stella Esther Mugasha aliyeapishwa kuwa Kamishna wa Tume ya Mahakama.

Prof Kabudi akila kiapo mbele ya Rais

Akizungumza baada ya kuwaapisha viongozi hao, Mhe. Rais Magufuli amewataka kuchapa kazi kwa juhudi, maarifa na kwa kutanguliza maslai ya Taifa na pia amewasihi kutobabaishwa na kauli ama vitendo vyovyote vya kuwavunja moyo.

Mhe. Rais Magufuli pia amewasihi waandishi wa habari na wamiliki wa vyombo vya habari kufanya kazi zao kwa weledi na kwa kutanguliza maslai ya Taifa badala ya kutoa kipaumbele katika masuala ya migogoro na mambo mengine yasiyo na manufaa kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

“Nchi yetu huko nje ina sifa kubwa sana, juzi tu hapa amekuja Rais wa Benki ya Dunia na amekubali kutupatia Shilingi Trilioni 1.74 na pia Benki ya Dunia ipo katika mchakato wa kutupatia fedha zingine Shilingi Trilioni 2.8 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo, haya ndio mambo muhimu ya kuandika lakini hebu angalia siku iliyofuata jinsi magazeti yalivyoandika” amehoji Mhe. Rais Magufuli.

Rais Magufuli akizungumza mara baada ya kuwaapisha viongozi hao

Aidha, amewaonya wamiliki wa vyombo vya habari ambavyo vimekuwa vikiandika habari za uchochezi na amemtaka Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe kuhakikisha vyombo vya habari vinafanya kazi kwa kufuata sheria na havitumiwi kuvuruga nchi.

Rais Magufuli (kushoto) akisalimiana na Dkt. Mwakyembe

Kabla ya kuwaapisha viongozi hao, Mhe. Rais Magufuli amepokea hati za utambulisho za Mabalozi 6 walioteuliwa kuziwakilisha nchi zao hapa nchini. Nchi hizo ni Cyprus, Bangladesh, Nepal, Ecuador, Newzealand, na Jamhuri ya Kongo.