Jumatatu , 25th Sep , 2017

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe amelipongeza Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kwa kuhifadhi vizuri kumbukumbu za Mashujaa wa Tanzania waliopigana vita na kusaidia ukombozi katika baadhi ya nchi za jirani.

Pongezi hizo amezitoa leo Mkoani Mtwara alipotembelea maeneo ya kumbukumbu ya kitaifa ambapo kwa Mkoani hapo ametembelea eneo la Mashujaa lililopo Nailendele lengo likiwa ni kujionea maeneo yaliyoweza kuhifadhiwa kumbukumbu zake za ukombozi wa Bara la Afrika ikiwemo mahitaji ya ziada ya maeneo hayo.

“Tunakipindi kifupi kuhakikisha kuwa kumbukumbu zote tulizonazo tunazihifadhi, tunaandika historia yetu sisi wenyewe Waafrika badala ya kuandikiwa na waliotutawala huko nyuma kwa ushahidi tulioutafuta wenyewe”, amesema Dkt. Mwakyembe.

Mhe. Mwakyembe ameongeza kuwa kazi kubwa inafanyika katika kuyatembelea maeneo hayo ili kujua kumbukumbu za maeneo hayo ikiwemo kuongea na mashuhuda wa matukio ya kumbukumu za maeneo husika kwa ajili ya kuandika historia ya Afrika.

Aidha Waziri ameipongeza JWTZ kwa kazi kubwa ya kuhifadhi baadhi ya maeneo ya kumbukumbu za kitaifa, jambo ambalo litarahisisha utunzaji wa kumbukumbu hizo kwa ajili ya Mradi wa Ukumbozi wa Bara la Afrika.