Jumatatu , 20th Feb , 2017

Watu wawili wamefariki dunia wakiwa kanisani katika ajali ya mvua iliyokuwa na upepo mkali huku wengine 26 wakijeruhiwa, wilayani Magu mkoani Mwanza.

Picha: Maktaba

Tukio hilo limetokea jana jioni katika Kijiji cha Lubungu, wilayani Magu mkoani Mwanza ambapo watu hao wametambulika kwa majina ya Ngwaku Nkulumbi (55) ambaye ni mwanamke na mtoto wa kike  Migayi Herenico (12)

Taarifa ya Jeshi la Polisi mkoani humo imeeleza kuwa tukio hilo limetokea baada ya upepo mkali kuezua paa la kanisa la dhehebu la Roman Catholic wakati waumini wa kanisa hilo wakiendelea na ibada.

Taarifa hiyo imesema kuwa , kati ya majeruhi hao 26, majeruhi 7 hali zao bado siyo nzuri wamepelekwa hospitali ya rufaa ya Bugando kwa matibabu zaidi huku majeruhi 17 wakiendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya wilaya ya magu na majeruhi 02 tayari wameruhusiwa.

Ahmad msangi - RPC mwanza

Jinsi ilivyokuwa.....

Inasemekana kuwa ibada hiyo ilikuwa imehudhuriwa na zaidi ya waumini 100, lakini ilichelewa kuanza kwa sababu Padre wa Kanisa hilo aitwaye Michael Kumalija miaka 60 ambaye  alikuwa ameanza kuhudumia katika kanisa la jirani alichelewa kufika kanisani hapo.

Padre huyo alifika majira ya saa 9 Alasiri, na dakika chache baada ya ibada kuanza, mvua kubwa iliyoambatana na upepo ilianza kunyesha.

Aidha inadaiwa kuwa baada ya tukio hilo kutokea waumini walianza kukimbia kutoka nje ya kanisa huku kila mmoja akijaribu kunusuru maisha yake, ndipo baada ya tukio hilo kupita iligundulika kuwa watu wawili wamefariki dunia