Ijumaa , 26th Mei , 2017

Mwanamume mmoja mkazi wa Mahina wilayani Nyamagana mkoani Mwanza amemuua mkewe kwa kumpiga risasi na yeye mwenyewe kujiua baada ya kutokea ugomvi baina yao.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza DCP Ahmed Msangi amewataja watu hao kuwa ni Maximilian Ngedere (40) na Tedy Patrick (38) ambapo ugomvi baina yao ulianza baada ya wawili hao kurudi kutoka katika biashara zao, majira ya saa 4:15 usiku wa tarehe 25 Mei, 2017.

Inadaiwa kuwa wawili hao ambao ni wafanyabiashara ya samaki walipofika nyumbani ulitokea ugomvi na pindi ugomvi huo ukiendelea kulisikika milio ya risasi kutoka chumbani.

Kamanda Msangi amesema Max alimjeruhi mkewe kwa kumpiga risasi sehemu ya mgongoni, kisha kujipiga na yeye mwenyewe risasi ya kifuani, hali iliyopelekea yeye mwenyewe kufariki dunia papo hapo huku mkewe akijeruhiwa na kukimbizwa hospitali ya rufaa ya Bugando akiwa na hali mbaya na ilipofika leo majira ya saa 3 asubuhi, akafariki dunia.

Amesema chanzo cha mauaji hayo bado kinachunguzwa na kwamba polisi wapo katika upelelezi kuhusiana na mauaji hayo wakati miiliyao ikiwa imehifadhiwa katika hospitali ya rufaa ya Bungando kwa uchunguzi zaidi.

DCP Ahmed Msangi