Jumatatu , 20th Feb , 2017

Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kushirikiana na daktari bingwa wa upasuaji wa watoto kutoka Falme za Kiarabu kwa mara ya kwanza wamefanikiwa kufanya upasuaji mkubwa wa mfumo wa chakula na njia ya haja kubwa kwa njia ya matundu madogo.

Madaktari bingwa Hospitali ya Taifa Muhimbili wakiendelea na zoezi la upasuaji wa tumbo kwa njia ya matundu.

 

Hayo yameelezwa leo na Daktari Bingwa wa upasuaji kwa watoto kutoka hospitali hiyo Dkt. Zaituni Bohari wakati wa zoezi la upasuaji huo ambao wamefanyiwa watoto wenye umri wa miaka 10 kutoka Zanzibar na Tanzania Bara na kuongeza kuwa wanategemea huduma hiyo kuanza kuifanya kwa watu wazima pia.

Amesema zoezi hilo litafanyika nchini kwa muda wa siku tano na wanategemea kuwafanyia watoto takribani 6 na kwamba njia hiyo ya upasuaji inapunguza gharama ya kusafirisha wagonjwa kwenda nje ya nchi kupatiwa matibabu kama hayo ambayo yalikuwa hayatolewi nchini huku akisema pia sasa bado hawajaweka bei elekezi ya huduma hiyo.

Amesema upasuaji huo hufanyika kwa muda wa saa zisizopungua nne kulingana na ukubwa wa tatizo hivyo ni wajibu sasa kwa kila mwananchi pindi aonapo hali isiyo ya kawaida katika mwili wake aende hospitali kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi zaidi nbadala ya kusubiri tatizo kuwa kubwa.