Jumanne , 29th Sep , 2020

Mgombea Urais kupitia Chama cha Demokrasia Makini Cecilia Mmanga, amesema iwapo Watanzania watampa ridhaa ya kuwaongoza, atahakikisha vijana wote wanaozurula mjini bila kazi, wanapelekwa kijijini na kila mmoja anapewa hekari moja ya shamba ili ajikite kwenye shughuli ya kilimo.

Mgombea urais kupitia chama cha Demokrasia Makini, Cesilia Mmanga.

Kauli hiyo ameitoa wakati akizungumza na EATV, na kuongeza kuwa Taifa la Tanzania lina vijana wengi hivyo ni lazima nguvu kazi iliyokuwa ikitumika wakati wa Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere inarudishwa katika kilimo.

Taifa letu lina vijana wengi, na kila kijana tutamkatia heka moja kwa sababu vijana wengi tunaona wako mjini wanazurula bila kazi maalumu, lakini tukipata ridhaa ya kuingia madarakani hawa vijana wote wasiokuwa na kazi tutawapeleka vijijini na kuwapa mashamba ili wafanyie shughuli za kilimo,” alisema Cecilia.

Aidha, Cecilia ameongeza kuwa wote watakaozalisha malighafi, serikali yake haitowapangia bei bali itawapa uhuru wa kila mmoja kuwa na bei yake ya mazao kwa kuwa wakulima ndiyo wanaojua jinsi wanavyohangaika.