Jumatatu , 20th Feb , 2017

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo na Mbunge wa Jimbo la Hai mkoani Kilimanjaro Mhe. Freeman Aikael Mbowe, leo alasiri amejisalimisha katika Kituo Kikuu cha Polisi Jijini Dar es Salaam.

Freeman Mbowe

Mbowe alitakiwa kuripoti kituoni hapo kwa ajili ya mahojiano kuhusiana na sakata linaloendelea la vita dhidi ya dawa za kulevya.

Taarifa iliyotolewa na chama hicho kupitia mtandao wake wa twitter ilisema "Mh. Freeman Mbowe amekamatwa na polisi waliokuwa wakimfuatilia alipokuwa anaelekea kituo cha polisi kati, mawakili wetu wa chama wako nae".

Taarifa zinadai kuwa Mbowe alishushwa kwenye gari yake akiwa njiani kuelekea polisi, na kupandishwa kwenye gari ya polisi, ambapo baada ya mahojiano kituoni hapo alipelekwa nyumbani kwake kwajili ya kufanyiwa ukaguzi.

Taarifa za kujisalimisha kwa Mhe. Mbowe zimethibitishwa na Msemaji wa Chadema Bw. Tumaini Makene ambaye hakutoa taarifa za undani wa nini kinaendelea hivi sasa ingawa kuna taarifa kwamba baadhi ya viongozi wa juu wa Chadema wanakutana katika kikao cha dharura kujadili suala hilo.

Baadaye majira ya alfajiri, uongozi wa chama hicho kupitia kwa Naibu Katibu Mkuu Salum Mwalimu, ulitoa taarifa za kuachiwa kwa mwenyekiti huyo wa CHADEMA

"Tunapenda kuwatangazia wanachama wetu, wadau,wapenzi na wapenda haki, amani na demokrasia ya kwamba Mwenyekiti Freeman Mbowe ameachiwa huru punde tu mnamo majira ya saa saba na robo usiku huu". Imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi Simon Siro ndiye aliyetoa wito wa kumtaka Mhe. Mbowe kuwasili kituoni hapo, ikiwa imepita takribani wiki mbili tangu jina la kiongozi huyo wa Kambi ya Upinzani Bungeni kuwa ndani ya orodha ya watu sitini na tano ambao Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Paul Makonda amewataka waende kituoni hapo kwa ajili ya mahojiano.

Hata hivyo siku chache baada ya jina lake kutajwa, Mhe Mbowe alikutana na wanahabari nje ya ukumbi wa Bunge mjini Dodoma na kukana kujihusisha na dawa za kulevya, huku akiweka wazi kuwa kamwe asingekwenda kituoni hapo kwa agizo la Mkuu wa Mkoa bali kwa agizo la Kamanda wa Polisi ambaye kwa maelezo yake ndiye mwenye mamlaka kisheria ya kumwita na kumhoji.