Jumatano , 22nd Feb , 2017

Mwanadada Agnes Gerald 'Masogange' amepandishwa kizimbani leo katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashitaka ya kutumia dawa za kulevya.

Agness Gerald 'Masogange'

Mrembo huyo ambaye ni maarufu kwa kupamba video za muziki wa wasanii wa Bongo fleva, amesomewa mashtaka mawili ya kutumia dawa za kulevya, makosa anayodaiwa kufanya aliyoyatenda Februari 2 mwaka huu katika Jiji la Dar es Salaam.

Akisoma mashtaka na wakili wa serikali, Costantine Kakula katika shtaka la kwanza alidai kuwa mshtakiwa alitumia dawa aina ya Heroine jambo ambalo ni kosa, na shtaka la pili ni kutumia dawa za kulevya aina ya Oxazepan, makosa ambayo mshtakiwa Agnes Gerald ameyakana.

Mara baada ya kusomewa mashtaka yake, ameachiwa kwa dhamana ya wadhamini wawili pamoja na kusaini bondi ya shilingi milioni 10.

Upelelezi wa shauri hilo balo haujakamilika na kesi hiyo itasikilizwa tena Mahakamani hapo tarehe 21 mwezi wa 3 mwaka 2017 na kwamba mshtakiwa hatatakiwa kuondoka nje ya Mkoa wa Dar es Salaam kwa muda huo licha ya kupewa dhamana.

Pia mrembo huyo amewahi kukamatwa nchini Afrika Kusini akihusishwa na usafirishaji wa dawa za kulevya mwaka 2013.