Jumatatu , 8th Mar , 2021

Msemaji Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi amesema kuwa utekelezaji wa miradi ya maji na usimamizi wake umeleta mafanikio kwa huduma ya maji nchini.

Msemaji Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi

Dkt. Hassan Abbasi amebainisha hilo leo Machi 8, 2021 alipozungumza na vyombo vya habari ambapo amesema ubora wa huduma za maji nchini umeongezeka kutoka wastani wa 47% kwa vijijini na wastani wa 74% kwa miji mikuu.

Sambamba na ubora huo Dkt. Hassan Abbasi amesema mapato yatokanayo na huduma za maji taka na maji safi pia yameongezeka.

''Katika mamlaka mbalimbali miaka mitano iliyopita mapato kwa mwaka yaliyokuwa shilingi bilioni 176.87 sasa yameongezeka hadi zaidi ya shilingi bilioni 301 kwa mwaka,'' amesema Dkt. Hassan Abbasi.

Katika ujumbe wake wa kilele cha Siku ya Wanawake Dunia leo ambapo East Africa Television (EATV) na East Africa Radio zinamtambua Mwanamke kama Kinara katika jamii Dkt. Abbasi amesema, ''Leo ni Machi 8, Siku ya Wanawake Duniani, kwa niaba ya Serikali tunawatakia wanawake wote wa Tanzania heri ya siku hii na waendelee kufanya tafakuri juu ya mchango wao zaidi kwa taifa na dunia. Tunawapenda sana''.

Aidha ameongeza kuwa, ''Wanawake wameendelea kuvunja rekodi ya kushika nafasi kubwa za kiuongozi hapa nchini akiwemo Mama Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Tanzania, na Eng. Zena Ahmed Said ambaye kwa sasa ni mwanamke wa kwanza kuwa Katibu Mkuu Kiongozi katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar''.