Ijumaa , 27th Mei , 2022

Mkuu wa wilaya ya Bariadi Lupakisyo Andrea, amesema kwamba katika oparesheni ya kuwaangamiza Fisi wilayani humo, wengine wamekuwa wakiwakuta na shanga, huku mapango wanayokaa Fisi hao wakikuta kuna mafiga, vyungu na nyama ambazo zimemalizika kuliwa.

Fisi

Hayo ameyabainisha mbele ya Kaimu Kamishna wa Uhifadhi wa Idara ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Mabula Misungwi Nyanda, aliyefika mkoani Simiyu kwa ziara ya kikazi, ambapo amepata wasaa wa kutembelea familia na kuwafariji watoto walioshambuliwa na kuumizwa na fisi hivi karibuni.

"Kwahiyo ni kweli wana shanga (Fisi), ukiingia mule ndani kwenya mapango yao utakuta mawe, chungu na nyama ambazo zimetoka kuliwa wakati huo, Mkuu tutaomba utuvumilie, tutajitahidi sana kufuata utaratibu lakini kama wana madhara kwa ulivyojionea, hawa tutaomba tuwaue, tukiweka mtego wa Mbuzi hawali, wanataka mtego wa mtoto ndiyo amle," amesema DC Andrea

Aidha akizungumzia kitendo cha Fisi hao kufika katika kituo cha polisi DC Andrea amesema, "Na kitu ambacho labda kiliwaudhi tuliua Fisi wa mwisho alikuwa na watoto, yaani Fisi anakwenda kituo cha polisi anajua kuna silaha hawa ndio wanatulinda, walipowaona Polisi na silaha zao wao wakaondoka,".