Ijumaa , 11th Aug , 2017

Licha ya kuwepo kwa shauhuku ya wananchi kuhusu matokeo ya kura ya urais Kenya  hali imekuwa tofauti baada ya wakenya kwenye mitandao ya kijamii kuunganishwa na picha ya mwanamume mmoja aliyekuwa akipata mlo wa Githeri kwenye foleni ya kupiga kura

Mpiga kura kutoka Kenya Bwana Martin Kamotho (41) 'Mr. Gither Man' mkazi wa Kayole,  Nairobi anatajwa kama kiunganishi cha amani kwenye uchaguzi wa Kenya huku akiandamwa na kampuni za chakula kupewa dili la ubalozi wa chakula baada ya kwenda kupiga kura akiwa na Makande (Mahindi na Maharage) kwenye mfuko wa plastiki.

Martin Kamotho alijizolea umaarufu alipopigwa picha akiwa na mfuko wa chakula cha mahindi na maharagwe (Githeri kwa lugha ya Kenya)  na kubandikwa jina la 'Githeri Man' akiwa kwenye foleni ya kupiga kura amekuwa akijadiliwa mitandaoni na  hata baada ya matokeo ya kura kutangazwa Wakenya wengi  wamekuwa wakimjadili huku vyombo vya habari vikiwa vinahaha kumpata.

Mr. Githeri Man akiwa kwenye foleni ya kupiga kura

Katika mahojiano aliyofanya na chombo kimoja cha habari nchini Kenya Bw. Martin Kamotho ambaye ni mfanyakazi wa usafi wa kata amebainisha kuwa kwenda kwenye kituo cha kupiga kura akiwa na chakula hicho lengo lake lilikuwa ni kutimiza haki yake ya msingi.

"Mimi kazi yangu ni kufagia kisha nikipata kipato ndiyo familia yangu nayo inapata kula. Wakati wa kwenda kupiga kura mimi nilibeba Githeri yangu na wakati nikiwa kwenye mstari wa chakula nilianza kumanga hapo kuna mtu nafikiri ndipo alipochukua picha".

"Nilisikia tu ni mtu amenipiga picha. Nikiwa mtaani nilikuwa nasikia kwamba nauliziwa na watu wa media nikiwa najiuliza kwamba kwa nini nimefanya kitu gani mbaya mpaka nataka kushikwa. Hata wakati nikiwa  nakuja hapa nilihisi napelekwa mahakamani" - Martin Kamotho

Kwenye Twitter picha ya mwanamume huyo ilihaririwa na kuwekwa katika hali ambazo ziliibua msisimko mkubwa na utani usio na kifani ambapo moja ya picha hizo ilionyesha akiwa katikati ya Rais Kenyatta, Makamu wa Rais William Ruto na vinara wa  NASA Raila Odinga na Kalonzo Musyoka.

Picha iliyohaririwa ikimuonyesha Mr. Githeri Man akiwa na viongozi wa Kenya.

Watu wengi walioonyesha kuguswa na 'Mr. Githeri Man'  lakini Daniel Ndambuki Mchekeshaji na muongozaj wa kipindi cha Churchill Show ambaye yeye alianza kumtafuta na kutaka na kumhomji mtu huyo kwenye kipindi chake pamoja na kumtafutia msaada wa kubadilisha maisha yake.

"Mimi niko tayari kumchangia pesa. Kubeba kwake githeri kunaonyesha alikuwa amejitolea kupiga kura. Amewaunganisha wakenya wote katika wakati wa taharuki. Tusherehekee maisha yake".

Bw. Martin Kamotho alinaswa na kamera ya mmoja wa wapiga kura aliyefahamika baadaye kwa jina la 'Ian Kinuthia' kijana  mwenye ndoto za kuwa mwanahabari, alimfuma akila mchanganyiko wake wa mahindi na maharage alioutia ndani ya mfuko ya plastiki katika siku ya kupiga kura Jumanne asubuhi  Agosti 8

Bw. Martini mpaka sasa ameshatafutwa na vyombo mbalimbali vya habari na makampuni ya vyakula , na ya mitandao ya simu Mr. Gither Man  tayari amepatiwa simu tatu za kisasa li kwendana na teknolojia.

Kuhaririwa kwa picha yake na kujadiliwa mitandaoni kwa Mr. Githeri Man  kumechangia wakenya mitandaoni kupunguza jumbe za chuki na kutulia kumfuatilia mtu huyo katika kipindi hiki cha uchaguzi.

Msikilize hapa Chini Mr. Githeri Man kwenye mahojiano.